KESI KUHUSU KUPINGA SHERIA YA VYOMBO VYA HABARI
LEGAL AND HUMAN RIGHTS CENTER NA KESI YA KUIPINGA SHERIA YA VYOMBO VYA HABARI katika Hali ya kuonyesha kutoridhishwa na upitishwaji wa sheria ya vyombo vya habari wanaharahakati mbalimbali wameamua kulipeleka suala hili mbele ya mahakama kwajili ya kuipinga sheria hiyo ya vyombo vya habari Tanzania, Kituo LHRC, MCT na THRDC waipinga Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari Mahakama ya Afrika Mashariki Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mapema Januari 11, 2017 kimeungana na Baraza la Habari Tanzania (MCT) pamoja na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kufungua shauri katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupinga Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari namba 12 ya mwaka 2016. LHRC kwa kushirikiana na MCT na THRDC wameamua kufungua kesi hiyo kwa lengo la kutaka baadhi ya vifungu vya sheria hiyo ambavyo vinakandamiza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza vifutwe kwani vinakiuka matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo zinataka nchi wanachama kuzingatia na kulinda haki ambazo zimeelezwa katika mkataba huo kwenye Ibara 6(d) na 7(2). Akizungumza na wanahabari mara baada ya kufungua kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2017, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania, Ndugu Kajubi Mukajanga ametanabaisha dhumuni la taasisi hizi kufungua kesi hiyo katika Mahakama ya Afrika Mashariki kuwa ni jukumu la kisheria iliyopewa mahakama hiyo katika kulinda haki kwa nchi wanachama na pia kiu ya kutumia mahakama hiyo ambayo haitumiwi na watanzania wengi mbali na kuwepo hapa nchini Tanzania. “Tanzania iliridhia kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2000. Chini ya Kifungu namba 23 cha Mkataba huo, Mahakama ya Afrika Mashariki imepewa mamlaka ya kutafsiri mkataba huo na kuhakikisha nchi wanachama wanaufuata na kusimamia”, amefafanua Mukajanga. Akijibu swali kutoka kwa wanahabari lililouliza kwa nini taasisi hizo hazikushiriki katika kutoa maoni na kusubiri hadi sheria hiyo kupitishwa, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Helen Kijo-Bisimba alisema “sisi (LHRC) na wadau wengine wengi hatukuridhishwa na muda uliotengwa na Kamati ya Bunge kwa ajili ya uchambuzi na utoaji wa maoni juu ya Mswada wa Huduma za Vyombo vya Habari na tuliiiomba Kamati iongeze muda ili kutoa nafasi ya ushrikishwaji wa wadau wengi zaidi na kufanya uchambuzi yakinifu utakaoleta sheria nzuri, lakini kamati haikuwa sikivu. Hivyo tumeamua kufungua shauri hili ili kutoa nafasi kwa mahakama kuchambua na kutoa maamuzi ya kisheria”. Kwa upande wake Mkurugenzi wa THRDC, Ndugu Onesmo Olengurumwa amewataka watanzania kujua kwamba malalamiko ya taasisi hizi yanawagusa watanzania wote, kwani madhaifu yaliyopo katika Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari hayaathiri uhuru wa vyombo vya habari pekee bali uhuru wa kujieleza kwa mtanzania mmoja mmoja. Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari namba 12 ya mwaka 2016 ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 5, 2016 na kuridhiwa na Rais Novemba 16, 2016. Katika kufungua kesi hiyo LHRC, MCT na THRDC wamewakilishwa na jopo la mawakili wabobevu akiwemo, Fulgence Massawe, Donald Deya, Jenerali Ulimwengu, Jebra Kambole, Fransic Stola na Mpale Mpoki.
Comments
Post a Comment